Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Madaba, Wakili Sajidu Idrisa Mohamed, amekutana na kufanya kikao na Watendaji wa Kata na Vijiji katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Madaba leo tarehe 02 Machi, 2026.
Katika kikao hicho, Mkurugenzi Mtendaji aliwataka Watendaji hao kwenda kufanya ziara katika maeneo yao ya kazi kwa lengo la kusikiliza na kutatua kero za wananchi kwa wakati. Alisisitiza umuhimu wa kuhakikisha miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika kata na vijiji inasimamiwa kikamilifu ili ikamilike kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.
Aidha, aliwahimiza kusimamia ipasavyo ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri na kuhakikisha yanaingizwa kwenye Mfumo wa Kielektroniki wa Ukusanyaji Mapato (FARS), pamoja na kuepuka matumizi ya fedha mbichi kinyume na taratibu za kifedha. Vilevile, aliwakumbusha kuzingatia na kuyaishi maadili ya utumishi wa umma katika utekelezaji wa majukumu yao kwa manufaa ya jamii.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Utumishi, Ndugu Hamza Mnaliwa, aliwakumbusha Watendaji hao umuhimu wa kufanya vikao vya kisheria katika kila kijiji kwa mujibu wa taratibu, kuhakikisha hali ya usalama inaendelea kuimarishwa, kusimamia matumizi sahihi ya fedha za umma, pamoja na kuwahi kufika ofisini kwa wakati na kutoa huduma bora kwa wananchi.
Kikao hicho ni sehemu ya jitihada za kuimarisha uwajibikaji, nidhamu ya kazi na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Madaba.
MADABA - RUVUMA
Anwani ya Posta: 38 BARABARA YA KIFAGURO MAGINGO, P.O.BOX 10, 57186 MADABA, SONGEA
Simu: 0252951052
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@madabadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Madaba.Haki zote zimeifadhiwa